Wasanii nchini wameiomba
Serikali kumalizia ujenzi wa ukumbi wa Sanaa za maonesho unaojengwa kwa
zaidi ya miaka minane sasa makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) eneo la Ilala sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza hilo
mapema wiki hii, wasanii hao walieleza kwamba kwa sasa kuna ufinyu wa
kumbi za za maonesho hali ambayo imekuwa ikiwafanya wasanii hao kukosa
maeneo ya kufanya sanaa zao hivyo kumalizika kwa ukumbi huo itakuwa ni
ahueni kubwa kwao.
“Ukumbi
huu ni muhimu sana kwetu, wengi tuliutazama kama mwanzo wa ufufuaji wa
Sanaa za majukwaani lakini sasa ni muda mrefu hauoneshi dalili za
kumalizika. Kuna kila sababu ya ukumbi huu kukamilika ili kutusaidia
katika maonesho yetu” alisema Msanii Khalid Kambau.
Kwa
upande wake msanii wa Sanaa za maigizo Christian Kauzeni ambaye pia ni
mwenyekiti wa chama cha wasanii waigizaji mkoani Dar es Salaam alisema
kwamba kutokana na ukumbi huo kutazamwa kama mkombozi wa wasanii kuna
kila sababu ya kuangalia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha unakamilika
mapema iwezekanavyo.
Awali
akiwasilisha mada kwenye Jukwaa hilo la Sanaa iliyohusu ‘Ubora wa
Filamu na Changamoto zake’ msanii na mzalishaji filamu maarufu nchini
William Mtitu alisema kwamba tasnia ya filamu chini imepata umaarufu na
kukua ingawa bado changamoto za uharamia, elimu na masoko zimeendelea
kuiathiri.
“Kwa
sasa filamu zinazozalishwa zimekuwa na ubora kuliko huko nyuma. Tatizo
liko kwenye elimu kwa wasanii, uharamia na masoko. Kulikuwa na maduka
zaidi ya sabini na tano yanayouza kazi za wasanii wa filamu lakini kwa
sasa yamebaki sita tu. Wengi wameamua kuuza kazi za nje mbazo ni nafuu.
Hii ni hatari” alisisitiza Mtitu.
Aliongeza
kwamba pamoja na Serikali kuirasimisha sekta ya filamu bado kuna
changamoto ya kazi zinazotoka nje kutokuwekewa stempu za mamlaka ya
mapato huku kukiwa na uharamia unaotishia bei za filamu halali zenye
stempu hizo.
Jukwaa
la BASATA limekuwa likifanyika kwa mwezi mara mbili siku za Jumatatu na
wiki hii kulikuwa pia na utambulisho wa asasi ya ubalozi wa Utamaduni
wa Mwafrika ambayo imeasisiwa nchini Cameroon, Afrika Magharibi mwaka
2014.
Msanii
na mzalishaji filamu nchini William Mtitu (Kulia) akiongea na wadau wa
Sanaa (hawako pichani) wakati akiwasilisha mada iliyohusu ‘Ubora katika
filamu na changamoto zake’ kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kushoto ni Katibu wa chama cha waandishi
wa habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli.
Rais
na mwanzilishi wa asasi ya Mabalozi wa Utamaduni wa Mwafrika (African
Culltural Embassy Association) Bwana Colpas Numfor kutoka nchini
Cameroon (Katikati) akionesha nyaraka mbalimbali za usajili wa asasi
yake wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya BASATA ya
Jukwaa la Sanaa. Kushoto kwake ni Katibu wa chama cha waandishi wa
habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli na Kaimu Mkurugenzi
wa asasi hiyo nchini Tanzania Bw. Maganiko Charles.
Msanii
maarufu wa Sanaa za majukwaani na maigizo Bakari Mbelemba maarufu kama
Mzee Jangala akifuatilia kwa makini mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa la
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kushoto kwake ni Rais
wa chama cha wacheza bao nchini Bw. Mande Likwepa.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza
akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyoibuka kwenye Jukwaa hilo la
Sanaa.
Afisa
Masoko kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Pastory John akitoa
maelezo mbalimbali kuhusu urasimishaji wa sekta ya filamu nchini kwenye
Jukwaa hilo la Sanaa.
Mdau
wa Sanaa na utamduni Bw. Francis Kaswahili naye alitoa mchango wake
kwenye Jukwaa la Sanaa. Alitoa wito kwa wasanii kuhakikisha wanakuwa na
kauli moja katika kuhakikisha wanasimamia maslahi yao.
Sehemu ya wadau wa Sanaa waliohudhuria Jukwaa la Sanaa wiki hii.
No comments: