NI uhakika asilimia 100 kwamba kiraka, Shomari Kapombe, ni mali ya Azam FC. Lakini kuna kitu kimoja kimemtokea mchezaji huyo ambacho kimeonyesha kwamba yeye ni jeuri na ana thamani kuliko Mrisho Ngassa wa Yanga.
Timu tajiri zaidi Tanzania na pekee Afrika Mashariki na Kati yenye uwanja binafsi ulioidhinishwa kwa michuano ya kimataifa, Azam FC, imenasa saini ya Kapombe kwa dau la Euro 47300 (Sh105 milioni).
Dau hilo la Kapombe limefuta rekodi ya Ngassa ambaye alikuwa mchezaji ghali zaidi wa kibongo kwenye Ligi ya Bara. Ngassa aliweka historia hiyo alipohamishwa kutoka Yanga kwenda Azam kwa dau la Sh 98 milioni mwaka 2010 kabla kwenda Simba kwa mkopo na baadaye kurudi Jangwani kwa dau la kawaida.
Kati ya kiasi hicho cha fedha za Kapombe, Euro 43000 (Sh95.8 milioni) zimeenda kwa klabu ya AS Cannes ya Ufaransa iliyokuwa na mkataba naye halafu asilimia 10 yaani Euro 4,300 (Sh9.5milioni) zitapelekwa Simba ikishapata uongozi mpya.
Chanzo makini cha Mwanaspoti ndani ya Azam, kilisema: “Tumeshatoa kiasi hicho cha fedha na sasa Kapombe yupo huru kuvaa jezi za Azam msimu ujao, hizo fedha za Simba zitachukuliwa na uongozi mpya utakaoingia madarakani kwani sasa tunawaacha waendelee na uchaguzi wao.”
Kabla ya usajili huo, Kapombe alianza kuonekana katika viwanja vya Azam Complex vilivyopo Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam akifanya mazoezi na jezi za timu hiyo na kuamsha hisia kwamba atajiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Ingawa Simba waliona hali hiyo wakapuuzia wakidhani ni masihara na kwamba kijana atarudi tu Msimbazi bila presha.
Kwa uhamisho huo, Kapombe anayemudu kucheza nafasi zote za ulinzi na kiungo katika timu, atavaa jezi ya Azam katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Kombe la Kagame na ligi kuu.
Huu ni usajili wa tano wa Azam baada ya hivi karibuni kuwasajili wachezaji wawili waliomaliza mkataba na Yanga ambao ni Didier Kavumbagu na Frank Domayo. Wengine waliosajiliwa na Azam hadi sas ni Ismail Diara wa Mali na Abdallah Kheri Salum kutoka Zanzibar.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments: