Kipa Juma Kaseja akiwa na cheti chake cha ukocha alichotunukiwa jana Ijumaa baada ya kuhitimu mjini Morogoro. Picha na Juma Mtanda
YANGA iko kwenye taratibu za kuachana na wachezaji wake mahiri ambao kuna uwezekano mkubwa wakatua Simba kwani baadhi yao wameshafanya mazungumzo ya awali Msimbazi. Wachezaji hao ni kiungo mwenye nguvu Athuman Idd ‘Chuji’, David Luhende, Juma Abdul na Ally Mustapha ‘Barthez’.
Lakini cha kushtua zaidi kipa mwenye heshima kubwa na rekodi ya aina yake nchini, Juma Kaseja yuko katika mazungumzo na uongozi wa Yanga akiwashawishi kusitisha mkataba wake wa mwaka mmoja kwa kile alichodai kwamba hana bahati na timu hiyo kwa sasa.
Kaseja ambaye hakuwa na wakati mzuri msimu uliopita jana Ijumaa alifuzu kozi ya awali ya ukocha na kupata alama ya daraja A katika mafunzo yaliyoanza Mei 5 mwaka huu katika Manispaa ya Morogoro.
Habari za uhakika kutoka kwenye kamati ya usajili zinasema Chuji anaachwa kutokana na nidhamu ndogo ingawa baadhi wanapinga na kusema kwamba ni mbadala mzuri wa Frank Domayo aliyesaini Azam.
Mbali na Chuji pia klabu hiyo imewachomoa Luhende na Abdul ambao awali waliudengulia uongozi wa klabu hiyo kuongeza mkataba huku Luhende ikiripotiwa kuwa amefanya mazungumzo na Simba ingawa hawana mpango nae sana kwavile aliwaringia awali wakafanya mazungumzo na Abdi Banda wa Coastal Union. Uongozi wa Simba umekiri kufanya mazungumzo na Barthez na watamalizana muda wowote.
Habari kutoka kwenye kamati ya usajili ya Yanga zinasema kuwa zaidi ya nusu ya wachezaji inaowahitaji imeshawapa mikataba mipya ambapo mchezaji wa mwisho alikuwa Mbuyu Twite. Kamati hiyo imepanga kupeleka baadhi ya wachezaji wenye mikataba kwa mikopo kwenye klabu zingine za Bara.
“Luhende Simba walimuhitaji kwa ada ya usajili ya Sh 6 Milioni na aichezee klabu hiyo ya Msimbazi kwa miezi sita lakini akagoma, alitaka aongezewe dau zaidi na Yanga pia aligoma kusaini yeye na Juma Abdul wote walikuwa mkumbo mmoja na Frank Domayo na Didier Kavumbagu,” kilisema chanzo chetu.
Habari za ndani zinadai kwamba Yanga ipo mbioni kuingia mkataba na Kelvin Edward wa JKT Ruvu na pia imepanga kuibomoa Mtibwa Sugar ingawa bado haijawekwa wazi ni kifaa gani.
Katika hatua nyingine, Mwanaspoti linajua kwamba mpaka jana Ijumaa Yanga ilikuwa imebaki na majina ya makocha watatu ambao ni kutoka katika nchi za Brazil, Uholanzi na Ujerumani. Habari zinasema kwamba majina ya makocha hao yapo kwa Mwenyekiti Yusuf Manji ambaye ndiye atakayefanya uamuzi wa mwisho kwani tayari kocha Hans Pluijm ameshatoa sifa za makocha hao kabla hajaondoka alfajiri ya leo Jumamosi.
Makocha hao imeripotiwa kwamba mmoja wao anafanya kazi nchini Ghana na ana uzoefu mkubwa na mazingira ya Kiafrika ambapo atatua nchini na mchezaji mmoja anayecheza nafasi ya kiungo.
Credit;Mwanaspoti
No comments: