NI mwisho wa zamani. Hakuna marefu yasiyo na mwisho. Juzi Jumapili inaweza kuwa siku ya mwisho kwa beki wa kushoto wa Chelsea, Ashley Cole, kuvaa jezi katika Uwanja wa Stamford Bridge baada ya nyota huyo kuondoka uwanjani hapo akiwa analia.
Cole, 33, alimwaga machozi wakati akiwaaga mashabiki wa Chelsea baada ya pambano la mwisho la Chelsea uwanjani Stamford Bridge dhidi ya Norwich City katika msimu huu wa Ligi Kuu England, mechi hiyo ilimalizika kwa timu hizo kutofungana.
Wiki ijayo Chelsea itacheza mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Cardiff City lakini itakuwa ugenini. Baada ya mechi dhidi ya Norwich, wachezaji wa Chelsea walizunguka uwanja wakiwaaga mashabiki wao na ndipo Cole alipoangua kilio kwa uchungu.
Baadaye beki huyo alibembelezwa na nyota wengine wawili wa Chelsea, Frank Lampard na John Terry, ambao nao hawana uhakika wa kuendelea kuwepo katika kikosi cha Chelsea msimu ujao baada ya kupoteza namba.
Cole amepoteza nafasi yake Chelsea baada ya kuporwa namba na Mhispaniola, Cesar Azpilicueta, ambaye licha ya kuanzia maisha yake katika upande wa kulia, alihamishiwa upande wa kushoto na kocha, Jose Mourinho na amekuwa akifanya vyema.
Cole mkataba wake utamalizika mwishoni mwa msimu huu na atakuwa huru kujiunga na timu yoyote anayotaka baada ya Chelsea kushindwa kumpatia mkataba mwingine.
Cole alijiunga Chelsea mwaka 2006 katika uhamisho uliokuwa na utata mkubwa, tangu hapo ameichezea Chelsea zaidi ya mechi 200 kwa mafanikio akitwaa ubingwa wa Ulaya, ubingwa wa Europa, mataji manne ya Kombe la FA na mawili ya Ligi Kuu England.
Kumekuwapo na uvumi kwamba nyota huyo amekuwa anatakiwa na Real Madrid ya Hispania huku pia akihusishwa kucheza katika Ligi Kuu Marekani ambako inadaiwa klabu ya New York Bulls inamhitaji.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, pia anadaiwa kumtaka beki huyo wa zamani wa Arsenal wakati huu upande wa kushoto wa timu hiyo ya Anfield ukiwa unalegalega tangu kuumia kwa Jose Enrique.
Chanzo Mwanaspoti
No comments: