Tuesday, March 11, 2014

MTOTO WA RAISI JAKAYA KIKWETE RITHIWAN KUWANIA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE TAARIFA KAMILI IKO HAPA.

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua, Ridhiwani Kikwete, kuwa mgombea katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, unaotarajiwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, uzinduzi wa kampeni za CCM utafanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Abdulrahaman Kinana na kufungwa na Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Alisema kampeni katika jimbo hilo zitaendeshwa na chama hicho ngazi husika na kuratibiwa na yeye mwenyewe Nnauye.
“Aidha kikao hicho cha Kamati Kuu, kilipokea taarifa ya maendeleo ya kampeni zinazoendelea huko Kalenga, huku ikisema imeridhika na mwenendo wa kampeni hizo, ambapo CCM inatarajia kupata ushindi,” alisema.
Katika uchaguzi wa kuwania nafasi hiyo ya ubunge Chalinze, Ridhiwani alishinda katika kura ya maoni kwa kupata kura 758, akifuatiwa na Shaban Madega kura 335, Athuman Maneno kura 206 na Changwa Mkwazu aliyepata kura 12.
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza rasmi mgombea wa ubunge katika Jimbo la Chalinze kuwa ni Mathayo Torongei.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Operesheni ya Uchaguzi Chalinze wa chama hicho, John Mrema, alisema Torongei alishinda nafasi hiyo ya kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho baada ya kuwamwaga wenzake watatu katika kura zilizopigwa na Kamati Kuu ya chama hicho juzi.
Alisema pamoja na ushindi huo wa kuthibitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, Torongei alishawamwaga wenzake hao katika kura ya maoni ya wanachama wa chama hicho, Jimbo la Chalinze kwa kupata kura 280 kati ya 478 ya kura zote zilizopigwa.
Wagombea wengine waliojitokeza katika uchaguzi huo ni pamoja na Francis Mgasa aliyepata kura 61, Frank Mzoo (23) na Mwenyekiti wa Jimbo la Chalinze wa chama hicho, Omary Mbambo aliyepata kura 84.
“Uteuzi wa mgombea huyu umefuata utaratibu wote za chama na Kamati Kuu imezingatia maoni na ushauri wa wanachama. Torongei ana historia nzuri na Chadema na tuna uhakika atashinda kwa kishindo Chalinze,” alisema Mrema.
Alisema chama hicho kimeamua kusimamisha mgombea katika jimbo hilo, ili kusaidia wananchi wa Chalinze kutatuliwa matatizo yao yaliyodumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Torongei aliwashukuru wanachama wa chama hicho Jimbo la Chalinze, kwa kumuamini na kumchagua na kuwaahidi kuwa endapo atashinda nafasi hiyo, atamaliza kero zao, hasa tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Mimi nimezaliwa na kukulia Chalinze, ni mtoto wa Chalinze na mtoto wa mkulima. Ninaifahamu vilivyo Chalinze kuliko mtu yeyote,” alijitapa.
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi-CUF kimemteua Fabian Leonard kuwa mgombea wake wa ubunge Jimbo la Chalinze.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya alitangaza hayo, makao makuu ya chama, Buguruni Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Kambaya alitamba kuwa CUF inakwenda kuchukua jimbo hilo na kwamba Leonard analijua vema jimbo hilo, kwani alishawania ubunge katika jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, ambapo alipambana na mgombea ubunge wa CCM, ambaye wakati huo alikuwa Rais Jakaya Kikwete.
“Huyu Leonard ni mzaliwa wa Chalinze na anayajua matatizo ya wana Chalinze. Alisisitiza kuwa Leonard amejipanga vyema na ana uhakika atashinda.
Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo la Chalinze, unatarajiwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vyama vya siasa vinapaswa kuwasilisha majina ya wagombea wao kesho kwa ajili ya kuthibitisha uteuzi wao. Kampeni rasmi za uchaguzi huo, zitaanza kesho kutwa.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo kufariki dunia.

No comments:

Speak Your Mind

Powered By Blogger · Designed By Seo Blogger Templates